Sunday, June 1, 2014

Shinyanga Kuongoza kwa utoro Mashuleni


MKOA wa Shinyanga umetajwa kuongoza kwa kuwa na watoto wengi wasiohudhuria shule ambapo hukimbilia katika uchimbaji wa madini.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika mafunzo ya waandishi wa habari, ilionyesha mkoa huo unaongoza kwa kuwa na asilimia 11 huku Jiji la Dar es Salaam likiwa na idadi ndogo ya asilimia 1.4.
Ripoti hiyo iliyotathimini yaliyojiri katika mwaka 2013 imeonyesha Mkoa wa Tabora unashika nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 10, Arusha asilimia 9.5, Singida asilimia 9.4 na Rukwa ikiwa na asilimia 8.5.
Iliitaja mikoa mingine kuwa ni Kigoma asilimia 8.4, Mara asilimia 8.0, Kagera asilimia 8.0 Mwanza asilimia 7.1 na Manyara asilimia 7.7.
Pia ripoti hiyo imeeleza sababu nyingine za watoto hao wanaoanzia miaka 7 hadi 16 kutoroka shuleni ni mimba za utotoni, umbali wa kutoka nyumbani hadi shule, ukosefu wa chakula shuleni na umasikini wa kipato kwa wazazi.
Hata hivyo, ripoti hiyo imeeleza kuwa katika tafiti waliyoifanya mkoani Tanga – Wilaya ya Korogwe katika Shule ya Msingi Mbuyuni walikuta ina wanafunzi 13 wa darasa la kwanza hadi la saba wakati ikipaswa kuwa na wanafunzi 262.

0 comments:

Post a Comment