Friday, June 13, 2014

BAJETI 2014/2015: Bajeti yawagawa wabunge, CCM waipongeza, upinzani waiponda





Dodoma. Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum imewagawa wabunge ambao baadhi wameipongeza, huku wengine wakiiponda.
Pamoja na kubana misamaha ya kodi, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alikosoa nyongeza ya kodi katika baadhi ya bidhaa akisema ni kuwabebesha mzigo wananchi.
“Nashukuru wamezingatia ushauri wetu wa kupunguza misamaha ya kodi, japokuwa hawakusema wataokoa shilingi ngapi, wangesema hilo.
“Pale bajeti inapokuwa na nyongeza ya kodi, lazima tufahamu kwamba mzigo huo utabebwa na wananchi, hilo halina ubishi.”
Mbunge wa Mkinga (CCM), Dunstan Kitandula alisema bajeti ni nzuri kwa sababu kwa mara ya kwanza haikugusa mafuta kwa kupandisha ushuru.  
“Ukigusa mafuta, umegusa eneo lote la uchumi na kwa bajeti hii kutakuwa na impact (matokeo) kubwa katika maisha ya kila siku ya wananchi kwa sababu kodi ya mafuta imebaki palepale,” alisema.
Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige alisema Serikali haikueleza itakakopata Sh19.8 trilioni ikizingatiwa kuwa katika bajeti inayomalizika Juni 30, mwaka huu imeshindwa kukusanya Sh18 trilioni hali iliyokwamisha shughuli nyingi za maendeleo.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) alisema: “Kwa kiasi fulani kuna unafuu kwa wananchi kwa sababu kodi ya Paye imepunguzwa na kitendo cha Serikali kusema itajenga reli ya kati kitasaidia kupunguza gharama za usafishaji.”
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema: “Bajeti haina jipya maana ni yaleyale ya mwaka jana ya nyongeza ya ushuru wa sigara na pombe.
“Imenukuliwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita, kilichobadilika ni style (mtindo) ya uandikaji, kama leo Watanzania wakiokoka sijui watapata wapi kodi na mimi ninaona kuongeza ushuru kwa pombe ni kushindwa kufikiri jinsi ya kuinua kilimo nchini.”
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alipongeza hatua ya kudhibiti magari ya mitumba akisema gharama zake ni kubwa na zinakaribiana na za magari mapya.
“Hatua hii ina manufaa, kwa sababu itatupunguzia magari chakavu kwani wanunuzi wa magari ya aina hiyo wanalazimika kulipa kodi ya uchakavu ambayo inasababisha gharama za gari husika kuwa sawa na kununua gari jipya,” alisema Azzan.

0 comments:

Post a Comment